Ijumaa , 27th Mar , 2015

Askofu wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, leo amejisalimisha kituo cha polisi kati, ili kuhojiwa juu ya kutoa lugha chafu dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Askofu wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Akiongea kabla ya kuhojiwa na polisi, Askofu Gwajima amejitetea kuwa alichofanya ni kutumia fursa ya kumuonya kiongozi mwenzake wa kiroho kutokana na kuwageuka wenzake katika makubaliano waliofikia katika tamko la kuipigia kura ya hapana Katiba inayopendekezwa.

Amesema kimsingi tamko hilo ambalo pia lilipinga kutungwa sheria ya kuanzishwa Mahakama ya Kadhi lilihusisha madhehebu yote ya Kikristo nchini, hivyo yalikuwa ni mapendekezo ya pamoja, hivyo kwa Kardinali Pengo kwenda tofauti nayo ni kupingana na maamuzi ya viongozi wenzake wa kiroho.

Hapo jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alimtaka Mchungaji Gwajima kujisalimisha kuhojiwa kufuatia kusambaa mtandaoni sauti na picha za video zinazomuonesha akimshambulia kwa maneno makali Kardinali Pengo.