Jumatano , 24th Dec , 2025

Watu tisa wamesalia hospitalini wakiendelea kutibiwa.

Idadi ya watu waliouawa katika shambulizi la kupigwa risasi katika baa moja nchini Afrika Kusini imeongezeka hadi kufikia watu 10 siku ya jana Jumanne huku polisi wakisema wamewatambua washukiwa wawili.

Wanawake watatu na wanaume saba waliuawa katika shambulio la siku ya Jumapili asubuhi, Disemba 21 katika kitongoji cha Bekkersdal, kilomita 46 magharibi mwa Johannesburg. Watu tisa wamesalia hospitalini wakiendelea kutibiwa.

Shambulizi hilo lilitokea mwendo wa saa 1 asubuhi, wakati takriban watu 12 wasiojulikana waliokuwa na bunduki kwenye magari mawili walipowafyatulia risasi wateja wa baa. Kwa mujibu wa Polisi, watu hao waliendelea kufyatua risasi ovyo huku wakikimbia eneo la tukio.

Meja Jenerali Fred Kekana, Kaimu Kamishna wa mkoa wa Gauteng, alisema watu wawili wametambuliwa kama washukiwa wa ufyatuaji risasi kulingana na ripoti ya polisi.

Msemaji wa polisi wa Gauteng pia amesema mmiliki wa tavern hiyo atashtakiwa kwa ulaghai na kuendesha duka la pombe haramu huku mamlaka ikitaifisha pombe zote kwenye baa hiyo.

Hii ni mara ya pili kwa tukio la kufyatuliwa risasi kwa wingi katika muda wa wiki tatu katika baa katika vitongoji nchini Afrika Kusini.

Mapema mwezi Disemba, shambulio la bunduki katika baa isiyo na leseni karibu na Pretoria liliua takriban watu 12, wakiwemo watoto watatu. Siku ya Jumatatu, mwanamume mwenye umri wa miaka 32 alikamatwa kuhusiana na ufyatuaji risasi huo.