Alhamisi , 11th Mei , 2023

Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, imedhamiria kuhakikisha inaboresha urithi wa kihistoria na malikale ndani ya wilaya hiyo.

Mkurugenzi wa Idara ya Malikale nchini Dkt. Christowaja Ntandu

Akizungumza kwenye kikao kazi cha kupokea taarifa ya namna mpango jumuishi wa matumizi ya maeneo ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara utakavyotekelezwa, Mkuu wa wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai, licha ya kuipongeza Wizara ya Maliasili kwa hatua nzuri inazozichukua za kuyainua maeneo hayo , ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za serikali katika uhifadhi endelevu wa maeneo ya Malikale yaliyo kwenye maeneo yao.

Mhe. Ngubiagai amesisitiza kuwa mpango wa matumizi ya maeneo ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ujikite pia kwenye kulinda majengo ya kale ya Kilwa Kivinje kwa vile majengo hayo watu wanarithishana kiholela huku Wizara ya Maliasili na Utalii iangalie zaidi katika uhifadhi wa mji wa Kilwa Kivinje.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Malikale nchini Dkt. Christowaja Ntandu, amesema kuwa ni mpango wa Wizara kupitia Idara anayoiongoza kuyaendeleza maeneo mbalimbali ya Malikale nchini ili yawe chachu ya maendeleo ya uchumi wa Taifa na wananchi kwa ujumla. 

Dkt. Ntandu ameongeza kuwa Kilwa ina utajiri mkubwa wa urithi wa Malikale na kupitia mpango madhubiti wa Wizara Kilwa sasa inakwenda kufunguka zaidi kiutalii hivyo amewashauri wakazi wa Kilwa wabuni mazao mengine ya utalii wa kiutamaduni ili kuongeza thamani ya Ultalii wa kihistoria  Kilwa.

Kikao hicho cha mpango jumuishi wa matumizi ya maeneo ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara (IGMP), kimehudhuriwa na Wataalam wa Malikale kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, maafisa wa idara mbalimbali za Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, madiwani na  viongozi mbalimbali wa ngazi za vijiji.