Jumatano , 21st Dec , 2022

Mamlaka ya Mawasiliano nchini - TCRA imesema ikifika Januari 31/2023 namba za simu ambazo hazitakuwa zimehakikiwa zitazuiliwa kupokea na kutoa huduma za Mawasiliano

Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesisitiza kuwa kila mtumiaji wa huduma za Mawasiliano anapaswa kutekeleza na kukamilisha kuhakiki namba zake za simu zinazotumika zilizosajiliwa kwa namba za kitambulisho cha uraia kabla ya Januari 31, 2023.

Mamlaka hiyo imeeleza kuwa, lengo la zoezi la hilo kuwa ni kumlinda mtumiaji wa huduma za Mawasiliano dhidi ya watu wanaojificha nyuma ya pazia la usajili wa watu wengine kutenda makosa yakiwemo ya utapeli kwa njia ya simu za kiganjani.

Imebainishwa kuwa baadhi ya watumiaji huduma za mtandao wa simu wamekuwa wakikwepa kusajili laini za simu kwa utambulisho wao kwa sababu mbalimbali, zikiwemo kukwepa kubainishwa kwa matendo ya jinai wanayotenda kwenye mtandao hivyo hutumia mbinu ya kununua laini za simu zilizosajiliwa tayari kwa utambulisho wa watumiaji wengine wa huduma za Mawasiliano ambapo TCRA imeeleza zoezi la uhakiki litawaondoa watu hao kwa kuwa mtumiaji husika mara atakapozibaini namba za simu zilizosajiliwa kwa namba za kitambulisho chake atazifuta kwa kuweka alama za kibayometria kwenye duka au wakala wa mtoa huduma wake wa Mawasiliano.

Mapema mwezi Novemba mwaka huu TCRA ilitangaza kuzifungia jumla ya namba tambulishi 52,087, zikiwemo zile zinazohusishwa na wizi, utapeli na ulaghai kupitia mitandao wa simu.