Alhamisi , 2nd Mei , 2024

Rais William Ruto wa Kenya amemteua Luteni Jenerali Charles Muriu Kahariri kuwa mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi uteuzi ambao unafuatia kifo cha aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Kenya Jenerali Francis Ogolla, aliyefariki kwa ajali ya ndege.

Luteni Jenerali Charles Muriu Kahariri, CDF Mpya wa Kenya

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Rais Ruto pia amempandisha cheo Meja Jenerali John Mugaravai Ornenda hadi cheo cha Luteni Jenerali na kumteua kuwa Makamu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.

Luteni Jenerali John Mugaravai Ornenda alikuwa Kamanda wa Jeshi la Wanahewa la Kenya kabla ya uteuzi huo.

Rais Ruto pia amemteua Meja Jenerali Fatuma Gaiti Ahmed kwa Jeshi la Wanahewa la Kenya na kumteua Kamanda wake na pia amemteua Meja Jenerali Paul Owuor Otieno kwa Jeshi la Wanamaji la Kenya na kumteua kuwa Kamanda.

Nafasi ya Mkuu wa Majeshi ya Kenya CDF inashikiliwa kwa msingi wa mzunguko na Majenerali ndani ya vikundi vitatu vya kijeshi ambavyo ni pamoja na Jeshi la Kenya, Jeshi la Wanahewa la Kenya na Jeshi la Wanamaji la Kenya

Jenerali Ogolla alikuwa kutoka Jeshi la Wanahewa la Kenya na Kahariri anatoka Jeshi la Wanamaji la Kenya.  

Wakati huo Rais William Ruto amewataka Wakenya wanaoishi katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko kuhamia maeneo salama ili kuepuka hasara zaidi ya maisha.

Rais alisema uchoraji wa ramani ambao umefanywa katika maeneo yanayokumbwa na maporomoko ya udongo na mafuriko unaonyesha kuwa baadhi ya Wakenya bado wako hatarini.

Rais aliyasema hayo katika alipowatembelea waathiriwa wa mafuriko. Baadaye alikagua shughuli za utafutaji na uokoaji katika eneo hilo.

Kufikia sasa, takribani watu 170 wamefariki, kutokana na mvua kubwa na maporomoko ya ardhi kote nchini Kenya.