
Waziri wa Nishati January Makamba
Katika maelezo yake Waziri Makamba amesema kampuni ya ETDCo imeonyesha udhaifu mkubwa kwenye utekelezaji wa miradi kadhaa ya kupeleka nishati vijijini ambapo ametoa mfano kwenye mkoa wa Mbeya kampuni hiyo kwenye mradi mmoja imefanya kazi kwa asilimi 28 tu hadi sasa.
"ETDCo leo hakuna kusaini mkataba wa mradi wa PERI Urban III, nendeni kwanza mkakamilishe kazi mkoani Mbeya na Katavi, nimeona kwenye mradi wa PERI Urban mmeshinda zabuni ya mkoa wa Kigoma na Geita na kazi zote hizo zina thamani ya shilingi bilioni 18," amesema Waziri Makamba.
"Hii si sawa na mmeshindwa kutekeleza miradi kwa wakati, mfano mkoani Katavi kwa kazi ile mlitakiwa hadi sasa walau mngekuwa mmefika asilimia 81 ya utekelezaji lakini bado utekelezaji upo chini," ameongeza Waziri Makamba.
Waziri Makamba amesema kuanzia sasa wakandarasi wa ndani watapimwa kwa utendaji (Performance) na si vinginevyo na kuongeza kuwa wakandarasi ambao utendaji wao ni wa mashaka, wasahau kupata miradi ya REA.
Wakati huo huo, serikali kupitia wakala wa Nishati Vijijini (REA) imesaini mkataba wa PERI Ubani Awamu ya Tatu, mradi huo una lengo la kupeleka umeme katika maeneo ya pembezoni mwa miji.
Mikoa ambayo imelengwa ni pamoja na Geita, Mtwara, Mbeya, Tabora, Tanga Singida, Kigoma ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy alisaini mikataba kwa niaba ya serikali na watendaji wa kampuni nne Jijini Dar es Salaam.
Kampuni hizo ni pamoja na Central Electricals International Ltd, DERM Electrics (T) Ltd, OK Electrical & Electronics Services Ltd na DIEYNEM Co Ltd.