Jumatatu , 19th Dec , 2022

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, amesikitishwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ambavyo ni moja ya kisababishi cha watoto kuishi katika mazingira hatarishi na kulaani vitendo hivyo huku akiwasihi wananchi wa Mwanza kuunga mkono juhudi za kupambana na ukatili.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja

Akizungumza katika hafla ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi iliyofanyika Kata ya Mabatini wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, amelaani vitendo hivyo na kuwataka wananchi wa Mwanza kuunga mkono juhudi za kupambana na vitendo hivyo.

"Hatuna budi kuhakikisha kwamba tunawaunga mkono wadau wote wanaoshiriki katika kutokomeza vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa hali na mali ili watoto wetu wawe na afya nzuri ya akili na wapate malezi bora," amesema Naibu Waziri Masanja 

Aidha, ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akishiriki katika kuwalinda na kuwatunza watoto hasa wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Hafla hiyo ilisaidia kupatikana kwa fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 1,890,000 zilizochangwa na wadau ambapo Mhe. Masanja alitoa fedha taslim kiasi cha shilingi milioni 1.5 kuchangia gharama za shule kwa watoto hao, na michango mingine iliyotolewa na wadau ni sabuni, sukari, unga wa lishe, madftari na kalamu.