Mauaji Kibiti, chanzo cha Mwandishi kupotea?

Thursday , 7th Dec , 2017

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Francis Nanai amesema kwamba japo hawana uhakika na sababu za kuchukuliwa na watu wasiojulikana kwa mwandishi wao Azzory Gwanda ila inawezekana hata kuandika habari za mauaji

yaliyokuwa yanatokea Kibiti ikawa chanzo.

Akizungumza na wanahabari leo wakati wakisisitiza kupatikana kwa mwandishi wa kampuni yao aliyepotea wiki mbili zilizopita huko Kibiti mkoani Pwani, Nanai amesema hawajui sababu maalumu ya kupotea kwa mfanyakazi wao ila wanachoamini wakimpata akiwa hai watapata sababu za kutosha.

"Siwezi kusema sababu za kupotea kwa ndugu yetu Azorry, lakini inawezekana kutokana na ripoti alizokuwa akizifanya kutokana na mauaji yaliyokuwa yakifanyika Kibiti ikawa sababu ya kukamatwa kwake, lakini pengine tukimpata anaweza kutupa mwanga wa sababu za kukamatwa kwake".

Aidha Nanai ameongeza kwa kusema kwamba Mwandishi wao Azzory hakuwahi kuripoti kuhusu kutishiwa amani au kufuatiliwa kwa namna yoyote ndiyo maana hawajui sababu ya kuchukuliwa na watu hao ni nini.

"Tishio lolote kwa mwandishi ni kuingilia uhuru wa habari, tukio la kutekwa kwa huyu mwandishi ni kuingilia uhuru wa vyombo vya habari. Kama kampuni hatujawahi kupata taarifa kama alikuwa anafuatiliwa au aliwahi kutishiwa maisha kutokana na kazi  alizokuwa anazifanya". Ameongeza.

Mbali na hayo Nanani ameomba ushirikiano kutoka kwa vyombo vya usalama wakiwepo Polisi katika kuhakikisha Azzory anapatikana huku akiwageukia waandishi wa habari kuendelea kudumisha ushirikiano waliouonyesha siku ya leo.

Azzorry Gwanda alikuwa mwandishi wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communication Ltd mwenye kituo cha kazi Kibiti- Pwani ambapo anadaiwa kuchukuliwa na watu wasojulikana tangu Novemba 21 mpaka leo hajulikani alipo.