Jumatatu , 10th Jun , 2019

Mbunge wa Singida Kaskazini Justine Monko amemtaka Kada wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Lazaro Nyalandu, asijifananishe na Mbunge Singida Mashariki Tundu Lissu na kueleza kuwa hawataweza kushinda majimbo yote Mkoa wa Singida.

Justine Monko ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na www.eatv.tv juu ya kauli ya Nyalandu kwamba chama hicho kitashinda Majimbo yote Mkoa wa Singida kwenye uchaguzi ujao wa mwaka 2020.

Mwandishi - "Mh. Nyalandu anasema watashinda majimbo yote ya Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Mbunge wa Singida Mashariki, vipi wewe haulihofii hili"?

Mbunge Justine Monko - "Mimi sihofii vitu vidogo kama hivyo kwa sababu moja tu,  umaarufu Nyalandu alikuwa nao wakati akiwa CCM, tangu amejiondoa hana nguvu hiyo, nguvu anayodhani alikuwa nayo ilikuwa ya CCM, na wala asijifananishe na Tundu Lissu, Nyalandu na Tundu Lissu ni vitu viwili tofauti kabisa."

Mwandishi  - "Umesema kuna tofauti kubwa kati ya Nyalandu, na Tundu Lissu labda Mheshimiwa tueleze tofauti yao ni ipi"?

Mbunge Justine Monko - "Hilo suala ningependa kulizungumzia siku nyingine, ila ninachoweza kusema kwa sasa tofauti ya Nyalandu na Tundu Lissu ni kubwa mno, huwezi kuwaweka pamoja, na hauwezi kulinganisha uwezo wa Nyalandu na uwezo Tundu Lissu."

Hivi karibuni akiwa mkoani Singida kwenye kampeni ya 'CHADEMA ni msingi' Lazaro Nyalandu alisema kupitia watu maarufu wa mkoa huo akiwemo yeye pamoja na Tundu Lissu watahakikisha wanashinda majimbo yote manne ya mkoa huo kwenye uchaguzi ujao wa 2020.