Ijumaa , 16th Nov , 2018

Baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kumfukuza bungeni Mbunge wa Mlimba, Susan Kiwanga (CHADEMA) kwa kile alichodai ni utovu wa nidhamu, amefunguka na kudai kuwa hawezi kujibishana na kiti cha kiongozi huyo.

Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freeman Mbowe.

Spika Ndugai alifikia uamuzi huo baada ya kukaa kwa muda akitaka vyombo vimsaidie kumpata mbunge aliyefanya utovu wa nidhamu wakati mbunge wa Tandahimba (CUF) Katani Ahmed Katani alipokuwa akitoa mchango wake.

Katani alikuwa akikanusha madai ya kujiuzulu akisema vyombo vya habari havikumtendea haki ndipo wabunge wa upinzani wakaanza kupiga kelele lakini Spika alipowanyamazisha wakaanza kuzomea.

Akizungumza na www.eatv.tv. Kiwanga amesema kuwa akiwa kama Mbunge mwenye jimbo, ana shughuli nyingi za kufanya jimboni kwake kuliko hata kuhudhuria vikao vya bunge, hivyo ameupokea uamuzi wa Spika Ndugai kwa mikono miwili.

"Wakati akichangia Mbunge wa Kinondoni Maulid Mtulia (CCM), wenzake walikuwa wanashangilia kwakuwa alikuwa akitusema upinzani kuwa tunamzuia Katani kujiuzulu, na ndio maana wakati Katani akiongea na sisi tuliamua kumshangilia ndipo mgogoro ulianzia pale", amesema Mh. Kiwango.

Mbunge wa Mlimba kupitia CHADEMA Suzan Kiwanga.

Akitoa amri kwa Mbunge huyo kutojihusisha na vikao au kamati za Bunge katika kipindi hiki na kuwa kama alikuwa kwenye orodha ya wachezaji wa Bunge anapaswa kuondolewa jina lake, Spika Ndugai alisema kuwa, "Nimejiridhisha kupitia vyombo vyangu, aliyefanya utovu wa nidhamu ni mheshimiwa Susan Kiwanga, sasa nakuomba utoke nje hadi bunge lijalo tutaonana Mungu akipenda Januari mwishoni mwakani", amemtaka mbunge.

Katika mkutano wa 13 huyu anakuwa mbunge wa pili kufukuzwa baada ya juzi Jumatano Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA) Mchungaji Peter Msigwa kufukuzwa na Naibu Spika Dkt. Tulia Akson baada ya kuambiwa alikuwa anapiga kelele.