Jumamosi , 28th Mar , 2015

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe amesema kelele zinazopigwa na nchi za Ulaya kuhusu uhusiano wa China na nchi za bara la Afrika zinatokana na uchu wa rasilimali zilizopo Afrika wakidhani China watanufaika nazo.

Bernard Membe

Membe Aliyasemana amesema hayo leo katika mahojiano maalumnu na vyombo vya habari katika kongamano la vijana wa vyama tawala vya siasa barani Afrika linalofanyika mkoani Arusha.

Amesema kwa muda mrefu sasa nchi hizo za Ulaya zimekuwa zikiupinga ushirikiano wa China na nchi za Afrika kwa madai mbalimbali ikiwemo kwamba China inazinyonya nchi hizo za Afrika jambo ambalo amesema si la kweli.

Amesema nchi hizo za Ulaya zimekuwa zikisema kuwa misaada ya fedha inayotolewa na China kwa nchi za Afrika imekuwa ikiziharibu nchi hizo kwakua hazina masharti kabisa au kuwa na masharti mepesi.

Ameeleza kuwa nchi za Afrika zimekuwa zikinufaika na misaada hiyo ya fedha kwakua imekuwa haina masharti magumu kwa kuwa haina riba kubwa na ina muda mrefu wa marejesho hadi kufikia miaka 10-15 na hata miaka 15-20.

Amesema kwa nchi hizo za Ulaya mikopo yao imekuwa na masharti magumu kwa kuwa na kipindi kifupi cha marejesho pamoja na vitisho vingi vinavyotolewa nan chi hizo ikiwemo kutishiwa kufungwa au kufungiwa misaada mingine pindi nchi itakaposhindwa kurejesha au itakapochelewesha marejesho.

Amesema kuwa nchi ya China imekuwa ikisaidia nchi za Afrika bila ubaguzi na kutolea mfano kuwa nchi ambazo zina matatizo ya mapigano, maradhi kama Ebola, matukio ya ugaidi na mengine mengi nchi hiyo imekuwa ikifika na kutoa misaada.

Amesema nchi nyingine za Ulaya zimekuwa na ubaguzi mkubwa ambapo zimekuwa hazifiki katika nchi zilizo na matatizo hayo na hata kufikia kuwaondoa watu na hata mashirika yao yanayojishughulisha na misaada mbalimbali.

Ametolea mfano wa misaada mbalimbali iliyowahi kutolewa na China ambayo ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa mpira wa Taifa, ujenzi wa kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mwalimu Nyerere, ujenzi wa reli na hata kituo cha mikutano cha umoja wa Afrika jambo ambalo hakuna nchi hata moja ya Ulaya iliyofanya hayo.