Jumatano , 27th Mei , 2020

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro ACP Salum Hamduni, amesema kuwa mara baada ya Mwalimu Agnes Mushi, anayetuhumiwa kumpiga mwanamke mwenzake kwa madai ya kwamba amemfumania na mumewe, kukiuka wito wa jeshi hilo, basi Polisi wataingia wenyewe kumsaka popote alipo na kumkamata.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, ACP Salum Hamduni.

Kamanda Hamduni ameyabainisha hayo leo Mei 27, 2020, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, na kuongeza kuwa mara baada ya kukamilisha upelelezi wale wote waliokuwepo eneo la tukio, ikiwemo wale walioshiriki kurekodi video na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii watafikishwa kwenye mkono wa sheria.

"Huyu mama hajaripoti, tunaendelea na ufuatiliaji wa mbinu nyingine ili kuweza kumfikisha kwenye vyombo vya sheria, sisi tunashughulika na jinai, na hatutarajii mtu kama anaweza kujipeleka Polisi, ni wajibu wa Jeshi la Polisi kumkamata, lakini kwa mwananchi aliyestaarabika ni vema anapopata taarifa za kutafutwa afike, inamuongezea credit hata uwezekano wa kupata dhamana na haki nyingine na tungemuona kama ni mtu ambaye anapenda kutii sheria" amesema Kamanda Hamduni.

Aidha akizungumzia kuhusu hali ya mwanamke aliyeshambuliwa kwa tuhuma hizo za kutembea na mume wa mtu, ACP Hamduni amesema kuwa alifanikiwa kupata PF3 na alienda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mawenzi.