Alhamisi , 5th Mei , 2022

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema kuwa serikali inaendelea kutafuta njia mbadala ambazo zitapunguza gharama ya maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,

Waziri Mkuu ametoa wito huo katika kikao kilichofanyika usiku wa kuamkia leo Mei 5, 2022, kwenye ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Oysterbay, jijini Dar es Salaam ili kufanya tathmini ya bei ya mafuta na kuangalia namna gani serikali inaweza kufanya ili kupunguza athari ya bei ya mafuta na kuleta unafuu wa gharama za maisha kwa Watanzania.

"Nawaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na waiamini Serikali yao kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha tunapunguza gharama za maisha kwa wananchi," amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema kikao hicho kimefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameagiza viongozi wa sekta husika wahakikishe wanatafuta suluhisho la kupanda kwa bei ya mafuta hata kama bei hiyo inaendelea kupanda duniani.

"Mheshimiwa Rais ameona changamoto wanayopitia Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, hivyo kikao hiki ni matokeo ya maagizo yake ya kuhakikisha sisi kama viongozi tunatafuta suluhisho la muda mfupi na la muda mrefu ili kukabiliana na changamoto hii," ameongeza

Waziri Mkuu amesema kuwa tayari Wizara ya Nishati imeanza kutafuta njia mbadala za uagizaji wa mafuta pamoja na kupunguza makato mengineyo ili kupunguza bei ya mafuta.