Jumatano , 11th Mar , 2015

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa, amelitaka Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuwafuata wateja na kuwafungia umeme, mahali wanapoishi badala ya kusubiri wateja kuwafuata .

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa.

Akizungumza jana katika ziara ya Kamati hiyo, iliyotembelea Kituo cha kupozea Umeme cha Njiro na kituo cha Kupozea Umeme kilichopo karibu na Uwanja wa Ndege wa KIA, Ndassa, amesema ni vyema sasa Tanesco ikafuata wateja mahali walipo badala ya wateja kuwafuata.

Amesema wateja wanaohitaji umeme ni wengi, hivyo ni vizuri Tanesco ikaboresha huduma zake kwa kuwafuata wateja walipo na kuwafungia umeme, ili kuongeza mapato badala ya hivi sasa wananchi kusota kufuata huduma hizo, huku baadhi ya mameneja na watumishi wasio waaminifu, wakila fedha za wananchi, kwa ahadi za kuwafungia umeme bila ya mafanikio.

Pia amesema ni vyema sasa Tanesco ikajitahidi kupata hati miliki za ardhi katika maeneo wanayopewa kwaajili ya kuboresha hali ya umeme sambamba na kuweka uzio unaostahili, ili kudhibiti baadhi ya watu wanaotaka kuhujumu miundombinu ya shirika hilo.

Naye Injinia Florence Gwang’ombe kutoka Tanesco Arusha,alisema mradi wa huo wa Electricity V-Pachage III, unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB ) kwa mkopo wa zaidi ya Sh. bilioni 72, unahusisha ujenzi wa njia ya umeme, wenye urefu wa kilomita 480 za msongo wa kilovoi 33.