Jumanne , 11th Dec , 2018

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira amesema kitendo cha bidhaa za Tanzania kushindwa kufanya vizuri kwenye masoko ya kimataifa ni kutokana na usaliti uliopo, na hivyo kusababisha mambo mengi kutoenda mbele.

Akizungumza na www.eatv.tv, Mama Mghwira amesema watu wanaotumwa kwenda kufanya kazi za kuitangaza Tanzania na kujifunza mapya ili walete tija nchini huwa wasaliti na kuishia kuangalia mambo yao binafsi, huku akitolea mfano wa zao la kahawa linalozalishwa mkoani humo kuwa ndiyo namba moja kwa ubora lakini haipo kwenye soko la dunia.

“Tanzania tunajisaliti wenyewe, wasaliti halisi wapo na walitangulia huko nyuma, walishindwa kulitetea taifa, mtu anaenda kwenye mikutano ya kimataifa ametumwa na nchi anaishia kwenda madukani kutembea kuona vitu, mambo ya kipuuzi kabisa, pole pole Tanzania inapotea, hatujui aliyemtuma anamfuatailia kiasi gani, na kila siku watu wanaenda nje wakirudi nyumbani hawafanyi”, amesema Mama Mghwira.

Mama Mghwira ameendelea kusema kwamba watu hao wakiwemo wawakilishi wetu ambao wana fursa kubwa ya kwenda nchi zingine mara kwa mara na kujifunza, huwa hawazingatii walichokiendea, na wakirudi wanashindwa kuwasilisha walichojifunza.

“Wawakilishi wetu ambao ni wabunge na wana dhamana kubwa, wana fursa kubwa sana ya kwenda nje kuona ili kuja nyumbani na kuboresha, lakini wanaishia kuja na kiatu kipya, tena akija anaringa nacho kweli, unaishia kuwahurumia tu”, amesema mama Mghwira.

Kutokana na hilo Mama Mghwira amesema anaandaa mfumo ambao utatangaza mkoa wa Kilimajaro na Tanzania kimataifa, ambao kila mkazi wa mkoa huo na wengineo watapata fursa ya kuutangaza kwa namna yake.