Jumanne , 18th Dec , 2018

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amebainisha kwamba kwa sasa serikali inaendelea kushughulikia madeni halali yakiwepo ya walimu ambayo tayari wameshaanza kulipwa.

Rais John Pombe Magufuli leo akiwa katika kikao cha Kamati Kuu (CC) ya CCM

Dkt. Magufuli amezungumza hayo mapema leo katika kikao cha Kamati Kuu (CC) ya CCM kilichokutana jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mafanikio yaliyofanyika kupitia CCM katika serikali ya awamu ya tano, Rais Magufuli amesema moja ya kazi kubwa iliyofanywa ni pamoja na kulipa madeni ya walimu ambayo yameshalipwa, madai ya wafanyakazi wengine na hata yale ya mifuko ya pensheni.

Ameongeza kwamba wakati anaingia madarakani alikuta serikali inadaiwa Trilion 3 kwenye mfuko wa pensheni lakini kupitia serikali yake wamepunguza mpaka kufikia takribani Bilion 200.

Pamoja na hayo amesema bado wanaendelea kufuatiia madeni mengine ikiwa ni pamoja na yale ya wasambazaji wa vitu mbalimbali mashuleni ambapo huko ndipo yalipo madeni mengine hewa ambayo yanapaswa kukomeshwa.