"Tutakuwa na siku 3 kumshukuru Mungu" - Magufuli

Jumatano , 20th Mei , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli  amesema kuwa nchi itakuwa na siku tatu za kumshukuru Mungu kutokana na hatua ya kuiepusha na janga la Corona.

Rais Magufuli

Amesema hayo akiwa njiani mkoani Singida akitokea wilayani Chato mkoani Geita, ambapo amesema kuwa ana imani baada ya siku chache janga la Corona litapotea nchini Tanzania na kubakia kuwa historia.

"Tutakuwa na siku tatu kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kumshukuru Mungu kwa maajabu aliyoyafanya katika taifa hili, ya kutuepusha na janga la Corona na nina uhakika katika siku chache Corona itapotea Tanzania na itabakia kuwa historia", amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa buidii na kwamba wasitishike na ugonjwa wa Corona bali wachukue tahadhari ya namna ya kuishi nao.

"Nchi yetu sasa inakwenda mbele sana, uchumi wetu unakua. Tanzania ni miongoni mwa nchi 5 Afrika zenye uchumi unaokwenda juu, zamani hapakuwa hata na mataa hapa Singida na hayo ni maendeleo kwahiyo tuendelee kuchapa kazi".

"Tusitishike tukubali kuishi nayo kwa sababu tumeshaishinda, na katika Mungu siku zote ushindi unakuwepo", ameongeza.