Jumatano , 4th Feb , 2015

WANANCHI wengi wa jamii ya wafugaji wilayani Hai, Mkoani Kilimanjaro, wanakabiliwa na uelewa duni juu ya umuhimu wa elimu, jambo linalosababisha kukwama kwa jitihada za Serikali za kuhakikisha watoto wenye umri wa kuanzashule wanapata elimu ya msingi

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga.

Hayo yamesemwa jana Wilayani Hai, katika mkutano mkuu wa kijiji cha Mtakuja kilichopo katika Kata ya KIA na Kaimu Afisa elimu wa wilaya ya hiyo, Makali Mahundi,alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji hicho.

Amesema kutokana na uelewa mdogo wa elimu, unasababisha baadhi ya watoto hao kuvunja vioo vya madirisha katika baadhi ya vyumba vya madarasa na kutoyatumia kabisa.

Makali amesema hali hiyo imechangia tatizo la watoto wa jamii hizo kutokupata elimu, hivyo inahitajika nguvu za ziada kutoka kwa wadau wa elimu, ili kuhakikisha wanafunzi wa jamii hiyo wanapata haki yao ya msingi.

Amesema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, wadau wa elimu wamelazimika kutoa elimu katika shule mbili za sekondari za kata zilizopo kwenye Halmashauri hiyo, ili waone umuhimu wa elimu na kusaidia shule hizo kuzikarabati.

Aidha Makali amesema shule hiyo iliyowekwa jiwe la msingi Mwaka 2009 na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimajaro,Mohamed Babu, wanafanya jitihada ili ianze mwaka huu kupokea watoto, shule ambayo ina ukubwa wa hekari
50 huku wananchi hao, wakiwa wamejenga madarasa manne.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga,amewataka wakazi wa kijiji hicho, kutambua kuwa urithi pekee wa watoto ni elimu, hivyo waunge mkono jitihada za Serikali, katika kuhakikisha watoto wanapata elimu.

Makunga amesema pia wamegundua shule ya Sekondari ya Tamnbarare, ilianzishwa kwa nguvu za wananchi ,lakini ilikuwa haijafanyiwa utaratibu wowote,ikabidi wahamasishe wananchi wakamilishe baadhi ya vitu,ikiwemo madawati,miundombinu ya maji,kuongeza matundu ya vyoo na hadi sasa tayari vimekamilika.

Mkuu huyo amesema Shule hiyo ilizinduliwa Mwaka 2009,lakini ilichelewa kusajiliwa, hivyo wameamua wanafunzi 25 waliofaulu mtihani wa darasa la saba na kukosa nfasi za kujiunga na kidato cha kwanza mwaka jana, waende kwenye shule hiyo.