Wafanyakazi waigomea serikali

Alhamisi , 6th Dec , 2018

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) limepinga kanuni mpya ya kukokotoa mafao ya wastaafu iliyotolewa hivi karibuni likisema inakandamiza wafanyakazi na kusema pendekezo lao lilikuwa ni kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii na si kanuni mpya ya vikokotoo inayolalamikiwa.

Pichani wafanyakazi wakiwa kwenye maandamano, lakini sio ya wakati huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kikao cha 35 cha shirikisho hilo mjini Morogoro, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya amesema kanuni hizo ni kandamizi na zimepokewa na wafanyakazi kwa mtizamo hasi na zitashusha ari yao na ufanisi.

Kuunganishwa kwa mifuko ni hoja ya TUCTA tangu mwaka 2004 lakini kanuni mpya ni kinyume cha mapendekezo yetu. Sisi tulitaka kanuni zibaki kuwa za mwaka 2017 ambapo kikokotoo ni 1/540 na mkupuo ni asilimia 50, huku wastani wa umri wa kuishi ukiwa ni miaka 15.5", amesema Nyamhokya.

Nyamhokya amesema hoja ya ufanisi wa mifuko kwa mkupuo wa asilimia 50 hakutakuwa na shida yoyote endapo serikali italipa madeni yote ya mifuko na mifuko kuacha uwekezaji usio na tija au kuuza kabisa.

Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imewahi kufafanua kuhusu deni hilo ikisema serikali haijakopa katika mifuko ya hifadhi ya jamii tangu mwaka 2013 kwa sababu tayari ilifikia ukomo ambao ni asilimia 10 kwa mujibu wa mwongozo.

Kwenye vitabu vya Serikali madeni yake kwa mifuko ya hifadhi ya jamii bado yapo. Serikali haijakana madeni yake tangu kuunganisha mifuko hii na mara ya mwisho ilisema itatoa hati fungani ili kulipa hayo madeni yake", amesema Irene Isaka.

Mjadala mkubwa unaendelea nchini baada ya kutangazwa kwa kanuni mpya za sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2014 ambazo zinaelekeza pamoja na mambo mengine, kuwa wastaafu wote watalipwa mkupuo wa asilimia 25 ya mafao pindi wanapostaafu na asilimia 75 inayobaki watakuwa wakilipwa kama pensheni ya kila mwezi.