
Akizungumza katika kikao cha kujadili namna ya kupandisha kiwango cha ufaulu na kutoa zawadi kwa walimu na shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya taifa, Kanali Sakulo amesema kuwa serikali haiwezi kuendelea kuwavumilia baadhi ya walimu ambao badala ya kuwa walezi wanakuwa chanzo cha kudidimiza ndoto za wanafunzi wa kike
"Zimekuwa zikijitokeza changamoto za hapa na pale kwamba mwalimu anatembea na mwanafunzi wake, hili serikali italivalia njuga, lazima hatua zichukuliwe maana yapo matukio ambayo yamekuwa yakijitokeza katika Wilaya yetu ya Missenyi na tumekuwa tukisema kuwa sehemu fulani kuna mwalimu amempa mimba mwanafunzi, ebu fikirieni matatizo mnayomsababishia huyo mtoto na familia yake" amesema Kanali Sakulo
Kwa upande wake afisa elimu sekondari katika Wilaya hiyo Maya Mbaraka amesema kuwa katika kipindi cha mwaka jana mpaka mwaka huu, wanafunzi nane wa sekondari wamepata mimba na kupoteza ndoto zao kimasomo, na kutumia fursa hiyo kutaja mikakati mbalimbali inayofanyika ili kukabiliana na mimba shuleni pamoja na utoro.
"Kuhusu masuala ya utoro na mimba shuleni tunaendelea kushirikisha bodi za shule ambazo pia hufanya vikao vya ndani lakini pia hukutana na uongozi wa shule na wazazi, lengo ni kupunguza vitendo hivyo ambavyo vimepungua kwa kiasi kikubwa hasa utoro" amesema Mbaraka.