Jumapili , 24th Dec , 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewatoa hofu wakazi 1,000 wa Manispaa ya Songea wanaoidai fidia ya sh. bilioni 3.8 ya eneo lao ambalo limechukuliwa na kuwa eneo la kiuchumi mkoani Ruvuma (Ruvuma SEZ) kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.

Mh. Majaliwa ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mwengemshindo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Manispaa hiyo ambapo amesema Serikali ya awamu ya tano inatambua kilio chao cha muda mrefu na kwamba alishawahi kupata ombi maalum kutoka kwa mbunge wao wa zamani, Bw. Leonidas Gama ambaye sasa ni marehemu.

Waziri Mkuu amewaeleza wakazi hao kwamba eneo hilo limetengwa na Manispaa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ambapo wawekezaji watatu tayari wamekwishajitokeza na wanataka kujenga viwanda vitatu.

Akitoa ufafanuzi kuhusu kuchelewa kwa malipo yao, Waziri Mkuu amesema kwamba kati ya wawekezaji hao watatu aliyekwishalipa fidia ni mmoja tu, na kwamba kwa mujibu wa sheria ya uwekezaji, fidia inapaswa kulipwa na mnunuzi wa eneo husika.

Kuanzia Juni 8-19, 2015, Serikali iliwalipa wakazi 1,179 sh. 1,920,242,121 ambapo kati ya hizo, sh. 1,210,078,261 zilikuwa ni malipo ya thamani ya mali za wananchi na sh. 710,163,860 zilikuwa ni riba kutokana na malipo hayo kuchelewa kufanyika.

Jumla ya watu 2,179 walifanyiwa tathmini mwaka 2008 na gharama yao kubainika kuwa ni sh. 3,254,737,622.