Jumatano , 4th Jan , 2023

Baadhi ya wanaume katika Halmashauri ya Shinyanga, wametajwa kuwa chanzo cha matukio ya ukatili wa kijinsia kwani wanatelekeza familia zao na kukimbilia maeneo ya senta kwenda kutafuta wanawake wanaokwenda vijijini kujiuza wakati wa mavuno na kusababisha familia kuwa maskini.

Senta

Licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kukomesha matukio ya ukatili wa kijinsia, baadhi ya wanaume wametajwa kuwa chanzo cha migogoro kutokana na kutelekeza familia na kuuza mazao hasa wakati wa mavuno na kukimbilia senta kutafuta wanawake wanaouza miili yao maarufu kwa jina la madada poa.

Nao baadhi ya viongozi wa Kata ya Nyida wamesema changamoto ya wanaume kutelekeza familia imepungua baada ya kupata elimu ya ukatili wa kijinsia.

Akizungumza kwenye mkutano wa jeshi la jadi sungusungu katika Kata ya Nyida Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akatoa maagizo kwa jeshi la jadi kuwafukuza wanawake wanaojiuza kwenye maeneo ya senta ambao wamepewa jina maarufu kama nzige.