Jumatano , 6th Jul , 2022

Mkuu wa wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya, amepiga marufuku tabia ya baadhi ya vijana wa jamii ya wafugaji wa kabila la Wasukuma kuwalazimisha wanawake kwa nguvu kufanya nao mapenzi na kutaka kuwaoa bila ridhaa yao na kuwaambia mila hizo za Chagulaga zimepitwa na wakati.

Mkuu wa wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya

Kauli hiyo ameitoa katika Kijiji cha Igumbiro katika mwendelezo wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi katika vijiji vya wilaya hiyo, jambo hilo liliibuka baada ya wanawake kutoa malalamiko yao kwake na kusema kuna baadhi ya wanaume wanalazimisha wanawake kufanya nao mapenzi ama kuwaoa bila ridhaa yao na hufanya hivyo kwa kuwavizia wakiwa wanaenda shambani au wakiwa kwenye minada.

"Suala la Chagulaga lilikuwa enzi za mabababu zetu huo ni ubakaji, kama umempenda mwanamke si uende ukazungumze nae, usione soo sema nae sasa unaenda kuvamia inaonesha mdomo wako ni mzito huna ujasiri wa kwenda kumtongoza mwanamke, domo zege," amesema DC Ngollo

Wananchi wanasema wanaume hao wakikutana na mwanamke humzunguka na kumwambia achague mtu mmoja afanye naye mapenzi, "Mwanamke akikataa anapigwa viboko kama kuna Baba yako au bwana wako akija anapigwa viboko na yeye"