Jumamosi , 11th Mar , 2017

Msanii wa bongo fleva Nay wa Mitego amemtaka msanii mwenzake Vanessa Mdee kuwa jasiri katika kipindi kigumu anachopitia cha kushikiliwa na polisi na kumtia moyo kwamba aone mambo hayo yanayomkabili ni changamoto za kufikia mafanikio.

Vanessa Mdee, Nay wa Mitego

Kupitia ukurasa wake wa Instagram leo asubuhi Nay amemtaka Vanessa kutokukata tamaa baada ya kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kujihusisha na biashara pamoja na matumizi ya dawa za kulevya  na kuongeza kuwa Mungu atamtia wepesi katika kesi hiyo.

“Amini hizi  ni changamoto tu na ni mapito ambayo binadamu tunapitia kwenye safari ya kuelekea kutimiza ndoto zetu, 'I pray for you my Friend' Vanessa Mdee. Naamini 'Brand' yako haiwezi kuharibika kirahisi kwa sababu umepambana sana, ni wasichana wachache wenye kuweza ku ‘fight’ kama wewe”. Nay aliongeza.

Nay ameongeza kuwa hafahamu Vanessa alipoanzia lakini ana imani kubwa kuwa amepambana kwa nguvu zote mpaka kufikia kuwa nembo kubwa yenye kutambulika na kwamba kama Mungu ndiye aliyemfikisha katika mafanikio hayo basi pia atamvusha katika changamoto hizo.

Pia Nay Amemsifia Vanessa kwa juhudi anazoonesha katika muziki wake ikiwa ni pamoja na kujivunia uwepo wake katika ‘game’ ya Bongo fleva.

Vanesa anashikiliwa na jeshi la polisi tangu Jumatano baada ya kuripoti kituoni hapo kama maagizo ya Mkuu wa Mkoa Paul Makonda yalivyomtaka baada ya kutajwa katika orodha ya watu wanaohusika na dawa za kulevya mwezi uliopita.