Jumatatu , 12th Oct , 2015

Kundi la kudansi la The WD watangazwa rasmi kuwa mabingwa wa mashindano ya Dance 100% 2015 baada ya kujivunia alama za kutosha na kujinyakulia zawadi ya ushindi shilingi milioni 5 sambamba na kombe kama ishara ya taji hilo.

Kundi la kudansi la The WD watangazwa rasmi kuwa mabingwa wa mashindano ya Dance 100% 2015 baada ya kujivunia alama za kutosha na kujinyakulia zawadi ya ushindi shilingi milioni 5 sambamba na kombe kama ishara ya taji hilo, wakifuatiwa na Team Ya Shamba walioshika nafasi ya pili na kujinyakulia shilingi milioni 1 wakifuatiwa na Best Boys Kaka Zao waliokamata nafasi ya 3 na zawadi ya shilingi laki 5.

Wakiongea baada ya kushinda taji hilo, The WD wameeleza kuwa wanafurahi sana kwa kuweza kubeba heshima hiyo kubwa, kuweza kupenya kutoka mchujo wa makundi shiriki yapatayo 50 yaliyoweza kujitokeza kwa mwaka huu, sambamba na kutoa shukrani kwa East Africa Radio na East Africa Television kwa kuwapatia jukwaa la kuonesha uwezo wao.
Mashindano hayo yalifanyika kwa raundi mbili, ya kwanza ikihusisha makundi kucheza muziki - megamix ambazo walitengeneza wenyewe zikibeba asilimia 40% ya jumla ya alama, huku mzunguko wa pili ukihusisha makundi hayo kucheza muziki walioandaliwa na kubeba alama 60%.

Makundi ya The Winners Crew waliokuwa wanawania taji hilo kwa mwaka wa tatu sasa na Team Makorokocho ambao ilikuwa ni mara ya kwanza kushiriki wanabaki katika rekodi kama washiriki walioweza kupambana kuingia katika fainali za mashindano hayo kwa mwaka huu.

Usikose kutazama eNewz kesho kujionea kwa undani matukio muhimu yaliyojiri katika fainali hizo mpaka kupatikana kwa mshindi na kumbuka, Dance 100% 2015 inadhaminiwa na Vodacom Tanzania na Cocacola, kinywaji rasmi cha Dance 100% 2015.