Upepo wa kisulisuli watua BAKITA

Jumatano , 16th Oct , 2019

Baada ya uwepo wa baadhi ya Video fupi, zinazotembea kwenye mitandao ya kijamii, zikimuonesha Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Moto, Mama Getrude Lwakatare, kuhusu upepo wa kisulisuli, Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA), limesema maana ya neno hilo ni upepo mkubwa unatokea ghafla.

Mchungaji wa Kanisa la mlima wa moto Gertrude Rwakatare

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, leo Oktoba 16, 2019, Msanifu Lugha Mkuu kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Consolata Mushi, ameielezea maana halisi ukiachana na ile ya kiimani, kupitia Kamusi sanifu ya Kiswahili Fasaha.

''Muktadha wa neno kisulisuli nikiangalia ni kwenye masuala ya imani, kumbukeni masuala ya imani kwao ni kusadiki jambo ambalo, hujaliona na kuliamini kwamba litatokana kama lilivyo kwa mujibu wa msamiati wa Kiswahili, neno Kisulisuli lina maana ya upepo unosafiri na kuzunguka na kwenda kwa kasi au kwa haraka'' amesema Consolata.

Aidha Consolata ameongeza kuwa, Mama Lwakatare alizungumza neno hilo katika muktadha wake na kumaanisha kwamba ni jambo ambalo litatokea kama kimbunga kwa sababu upepo wa aina hiyo hutokea ghafla.

''Kama yeye alitumia kama mchumba anaweza akaja kama upepo wa kisulisuli ni muktadha wa imani, kwamba wapo na watajitokeza bila kutarajia, sasa msije mkaiingiza kwamba atajitokeza anazunguka kama upepo Laa! hasha! muktadha uongozwe kwenye kupata maana ya maneno, kwamba umekwenda kanisani ni msichana ama mvulana bila mwenzio lakini pale baada ya sala na imani akatokea mwenzio hukutarajia, hukupanga'' ameongeza Consolata.