Ajibu awapigia magoti wanayanga

Ijumaa , 12th Jan , 2018

Baada ya kutolewa katika michuano ya kombe la mapinduzi kwa kipigo cha penalti 5-4 dhidi ya URA, Mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu Migomba ameomba radhi kwa mashabiki wa timu hiyo kutokana na matokeo hayo mabaya.

Mshambuliaji huyo  aliyetokea klabu mahasimu wao timu ya Simba SC na kutokea kuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga amesema hawakupenda kupata matokeo ya aina ile lakini ilitokea vile kwa sababu mpira una matokeo matatu.

Naomba mashabiki wetu wa Yanga watusamehe kwa matokeo mabaya hakuna timu ambayo inapenda kupoteza mchezo ila ndiyo imeshatokea na matokeo ndiyo hayo katika mpira kuna matokeo matatu tu, kusohinda, kufungwa na kutoka sare, chamsingi kwa mashabiki ni kutupa ushirikiano zaidi na kutuunga mkono katika michezo iliyo mbele yetu ,” amesema Ajibu.

Katika mchezo huo wachezaji ambao walipiga penalti ni Papy Tshishimbi, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Daud Raphael na Obrey Chirwa ambaye alikosa.

Yanga iliondolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi katika hatua ya nusu fainali na URA ya Uganda kutinga fainali itakayopigwa kesho usiku dhidi ya Azam FC ambayo nayo iliitoa Singida United kwa bao 1-0.

Yanga ilirejea Jijini Dar es Salaam jana ikitokea Zanzibar ikiwa ni siku mbili tu zimepita tangu mahasimu wao, Simba SC kutolewa na timu ya URA katika hatua ya makundi jambo ambalo mashabiki wa Yanga waliitumia kama fimbo ya utani kwa watani zao wa jadi na kuwatolea kejeli za kiutani lakini furaha yao ikaingia shubiri baada ya wao pia  kuondolewa mikono mitupu na timu iliyowatoa watani zao.