Jumatatu , 21st Oct , 2019

Uongozi wa klabu ya Azam FC leo imemtangaza kocha wake wa zamani, Aristica Cioaba, kuwa Kocha Mkuu mpya wa kikosi hicho.

Kocha mpya wa Azam FC, Aristica Cioaba (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat.

Cioaba ambaye ni raia wa Romania, aliifundisha Azam FC mwaka 2017 na sasa amechukua nafasi ya Etienne Ndayiragije ambaye ni kocha wa muda wa Taifa Stars.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari hii leo wakati wakimtangaza kocha huyo mpya na sababu iliyopelekea kumrejesha kocha huyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' amesema kuwa wamezingatia kumrejesha kocha huyo ili kuepuka kuwa na kocha ambaye haijui vizuri ligi na klabu hiyo.

"Tumeona ni bora kurudi na Cioba ambaye katika kipindi anatuacha, alituacha tukiwa tumebakiza mechi tatu za ligi na tukiwa nafasi ya pili na wakati ule alikuwa na kikosi ambacho hakina wazoefu", amesema Popat.

"Bodi ya wakurugenzi na uongozi wote kwa ujumla tumekubaliana kwa pamoja kocha anayefaa kurudi ni Aristica Cioaba", ameongeza.

Aidha ameitaja sababu ya kuachana na kocha Etienne Ndayiragije kuwa ni baada ya Shirikisho la Soka Tanzania TFF kuiomba klabu hiyo kumruhusu Ndayiragije ili achukue mikoba ya kuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars baaya ya mafaniko aliyoyaonesha hivi karibuni ikiwemo kufuzu michuano ya CHAN.