Jumanne , 9th Feb , 2021

Mabingwa wa bara la Ulaya, klabu ya Bayern Munich ya nchini Ujerumani imetinga hatua ya fainali ya michuano ya kombe la Dunia la vilabu baada ya usiku wa jana wa Februari 9, 2021 kuwafunga mabingwa wa bara la Afrika, klabu ya Al Ahly mabao 2-0 kwenye dimba la Al Rayyan nchini Qatar. 

Wachezaji wa Bayern wakishangilia baada ya kupata bao la kwanza usiku wa jana.

Mabao ya ushindi ya mchezo huo, yote yamefungwa na mchezaji bora wa Dunia wa FIFA wa mwaka 2020, Robert Lewandowski aliyefunga bao la kwanza dakika ya 17 na la pili dakika ya 85 na kuwakatisha matumaini ya kuiona fainali mabingwa hao wa kihistoria barani Afrika.

Mabao hayo yanamfanya mshambuliaji huyo hatari Duniani kwasasa, kufikisha mabao 29 na kutengeneza mabao mengine 7 katika michezo 27 aliyoichezea klabu yake ya Bayern Munich kwenye michuano yote tokea kuanza kwa msimu huu.

Ushindi huo unaifanya Al Ahly kupoteza nusu fainali yake ya tatu na kumruhusu Bayern Munich kutinga fainali hiyo kwa mara ya pili ndani ya miaka takribani saba baada ya mara ya mwisho kutwaa kombe hilo mwaka 2014 baada ya kuwa mabingwa klabu bingwa Ulaya mwaka 2013.

Bayern watacheza fainali hiyo na mabingwa wa bara la Amerika ya kaskazini, Tigres UANL ya nchini Mexico ambaye imetinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kuwatoa wababe wa nchini Brazil, klabu ya Palmeira kwa kuwafunga bao 1-0.

Mchezo wa fainali ya kombe la Dunia la vilabu utachezwa siku ya Alhamisi ya tarehe 11 Februari 2021, pamoja na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wa michuano hiyo ambapo Al Ahly ya Misri  atachuana na Palmeira ya Brazil.

Kama Bayern wakifanikiwa kubeba kombe hilo, basi watafikia rekodi ya mwaka 2008-09 ya FC Barcelona ya Hispania ya kutwaa mataji yote makubwa kwenye ngazi ya vilabu ndani ya msimu wao wa mafanikio baada ya Bayern kutwaa Bundesliga, DFB Pokal, klabu bingwa Ulaya na hata la Uefa Super Cup.