
Mshauri wa benchi la ufundi kwa timu za Zanzibar na Tanzania Bara katika michuano ya kombe la Chalenji nchini Ethiopia ambaye pia ni kocha wa timu ya taifa Taifa Stars Charles Boniface Mkwasa amesema, uendeshaji wa mashindano ya CECAFA bado haujawa madhubuti jambo linalonaweza kuchangia ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kudidimia na kushindwa kwenda na wakati, akitolea mfano ratiba zilivyopangwa katika hatua ya robo fainali katika michuano ya Chalenji inayoendelea nchini Ethiopia.
Mkwasa amesema, haijawahi kutokea katika michuano yoyote, timu zilizo kundi moja kukutana katika hatua ya robo fainali kama ilivyokuwa kwa Kill Stars ambayo ilikuwa ikiongoza kundi A lakini ikapangwa kukutana na Ethiopia ambayo ni kundi moja huku Sudan na Sudani Kusini pia wakiwa kundi moja wakakutana katika hatua ya robo fainali badala ya kukutana angalau katika nusu fainali au fainali.
Mkwasa amesema, suala lingine ambalo CECAFA walilifanya na hawakulielewa ni kwa upande wa wachezaji ambao walikuwa na kadi za njano ambapo CECAFA ilizifuta kadi za njano moja moja kwa wachezaji waliokuwa nazo huku wenye kadi mbili za njano zikaachwa kama zilivyo ambapo kwa upande wa Kill Stars kulikuwa na wachezaji wenye kadi za njano.
Mkwasa amesema, Kili Stars ilicheza vizuri katika michuano hiyo na ilionesha kiwango kizuri na hata wachezaji ambao hakuwahi kuwatumia Taifa Stars amewaona wakifanya vizuri lakini bado ni wadogo na wanahitaji muda mrefu wa kukomaa na kupata uzoefu ili kuweza kupata nafasi katika kikosi cha kwanza katika mashindano mbalimbali.
Kwa upande wa timu ya Taifa ya Zanzibar Mkwasa amesema, Timu hiyo haikuanza vizuri sana kutokana na matatizo yaliyotokea kwa upande wa Shirikisho la Soka Zanzibar ZFA na bahati mbaya alishindwa kuonana na timu siku ya kwanza kutokana na kupishana katika ratiba lakini alikutana nao katika mechi na kuifanyia timu tathimini ambapo mechi ya kwanza ilicheza vizuri.
Mkwasa amesema mechi ya pili kikosi cha Zanzibar Heroes kilishakata tamaa lakini alikutana nao na kuwapa ushauri ili kufanya vizuri mechi ya mwisho dhidi ya Kenya ambapo walijitahidi na kuweza kuibuka na ushindi licha ya kutolewa katika hatua ya makundi.