Jumatano , 24th Mar , 2021

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Wales, Gareth Bale amesema michezo ya kuwania nafasi ya kufuzu michuano ya kombe la Dunia itakayochezwa usiku wa leo huenda ikawa ndiyo ya nafasi ya mwisho kwake na baadhi ya wachezaji wenzake kutokana na kuwa na umri mkubwa.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Wales, Gareth Bale.

Bale mwenye umri wa miaka 31, amesema hawana budi kucheza kwa kupamba dhidi ya timu ya taifa ya Ubelgiji usiku wa leo ili kuweka hai matumaini yao ya kuandika historia ya kufuzu kombe la Dunia litakalochezwa mwaka 2022 nchini Qatar tokea Wales ifuzu kwa mara ya mwisho mwaka 1958.

Maneno hayo ya Gareth Bale yana maana kuwa, kama Wales ikishindwa kufuzu kombe la Dunia la mwaka 2022 nchini Qatar, huenda yeye na baadhi ya wachezaji wenzake wenye umri mkubwa watakuwa wamestatundika daruga na wakakosa kombe la Dunia la mwaka 2026 nchini Marekani.

Michezo mingine ya kufuzu michuano ya kombe la Dunia kwa mataifa ya bara la Ulaya itakayochezwa usiku wa leo ni pamoja na mchezo wa timu ya taifa ya Ureno ya Cristiano Ronaldo dhidi ya Azerbaijan na ule wa Serbia watakapokipiga na Jamhuri ya Ireland kutoka kundi A.