Jumatatu , 19th Feb , 2018

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe leo amethibitisha kuwa Rais wa FIFA Gianni Infantino atatua nchini Alfajiri ya Februari 22 kwaajili ya kuongoza mkutano mkuu wa mwaka wa FIFA na baadae kuonana na Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa leo Waziri Mwakyembe imeeleza kuwa Rais wa FIFA anatarajia kuwasili nchini usiku wa saa nane kuamkia Februari, 22 2018 ambayo ndiyo siku ya mkutano na saa tatu asubuhi yake ataelekea Ikulu kukutana na viongozi wakuu wa nchi.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Bw.Wilfred Kidao amesema mkutano huu wa viongozi wa FIFA na CAF umebeba ajenda mbalimbali  ikiwemo kujadili Maendeleo ya Soka la Wanawake, Maendeleo ya Soka la Vijana, Utaratibu wa kusaidia Vilabu vya soka pamoja na vipaumbele mbalimbali vya kukuza soka kwa nchi za Afrika.

Aidha Rais huyo wa FIFA anatarajia kuondoka nchini jioni mara baada ya kumaliza mkutano wake na kushiriki chakula cha jioni.