Mhilu amesema yupo tayari kurejea Yanga.

Jumanne , 30th Jun , 2020

Yusuph Mhilu amesema yupo tayari kujiunga na waajiri wake wa zamani klabu ya Yanga iwapo watapeleka ofa itakayokubalika kwa pande zote mbili.

Mshambuliaji machachari wa Kagera ,Sugar Yusuph Mhilu katika picha,wakati akisaini mkataba wa kuitumikia miamba hiyo ya mkoani Kagera.

Mshambuliaji wa klabu ya Kagera Sugar,inayoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara,Yusuph Mhilu ameifungulia mlango klabu yake ya Zamani ya Yanga,iwapo itahitaji huduma yake kwa mara nyingine.

Nyota huyoa ambaye ndiye kinara wa mabao kwa wachezaji wazawa katika ligi kuu Tanzania bara akiwa na mabao 13,amesema amesikia taarifa za kuhitajika na Yanga ingawa bado hajapokea barua rasmi ambayo anasisitiza kwamba hatosita kurejea mitaa ya Twiga na Jangwani kama nafasi itapatikana.

Mhilu ambaye alilelewa katika klabu ya Yanga ya vijana kwa miaka mitatu,na kupewa nafasi katika kikosi cha wakubwa na aliyekua kocha wa klabu hiyo Mwinyi Zahera,alishindwa kuendelea kuaminiwa baada ya kupelekwa kwa mkopo katika klabu ya Ndanda mnamo msimu wa mwaka 2018/19 kabla ya kujiunga na Kagera msimu huu.

Ndani ya msimu huu ,Mhilu amehusika katika mabao 17 ya Kagera Sugar ambapo amefunga 13 na kutoa pasi za mabao 4,na sasa ndiye mfungaji bora wa pili katika ligi kuu nyuma ya kinara Meddie Kagere wa Simba mwenye mabao 19 hadi sasa.

Hakuna mchezaji wa klabu ya Yanga ambaye amefikisha idadi ya Mhilu kiasi cha kuwafanya mabosi wake wa zamani kufikiria kumrejesha nyota huyo wa kitanzania.

Katika hatua nyingine mhilu amewashauri Yanga kuwa watulivu katika kipindi hiki wanachopitia huku akiamini wakijipanga wanaweza kurejesha makali yao waliyokua nayo kwa misimu kadhaa iliyopita