Ijumaa , 20th Mei , 2022

Mshambuliaji wa zamani wa Klabu ya Simba, ambaye kwa sasa anaitumikia Mtibwa Sugar, Deo Kanda amesema malengo yake ni kuhakikisha anarejea katika vilabu vikubwa vya soka hapa nchini Tanzania.

Deo Kanda akishangilia bao enzi akiitumikia Klabu ya Simba .

Kanda ambaye ni raia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, amesema yupo Mtibwa ili kupata muda mwingi wa kucheza utakaomuwezesha kurejea katika vilabu vikubwa japo hakuvitaja.

Nyota huyo aliyejiunga na Simba kwa mkopo akitokea TP Mazembe, amesema Tanzania ni sehemu sahihi kwake kucheza soka na kuna ushindani mkubwa jambo ambalo ana amini ndilo linawafanya wachezaji kutoka Congo kuamua kuja kucheza Ligi Kuu Tanzania bara.

''Nipo Mtibwa ili nipate muda wa kucheza mara kwa mara, ninahitaji kurejea kwenye vilabu vikubwa Tanzania''alisema Deo Kanda.

Katika hatua nyingine Kanda ameipa Klabu ya Yanga nafasi kubwa ya kuwa bingwa msimu huu kutokana na kujiimarisha zaidi ya timu nyingine.

''Ligi ni ngumu msimu huu,lakini kwa mwenendo ulivyo hata kama mechi za kucheza bado nyingi lakini ninaona Yanga itachukua ubingwa ''Deo Kanda.

Kuhusu kurejea Simba, Deo Kanda amesema yupo tayari kwakuwa ni timu aliyoitumikia hivyo iwapo watahitaji huduma yake hatosita kuwatumikia.