Jumatatu , 27th Jun , 2016

Klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa imetangaza rasmi kuachana na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Laurent Blanc ambaye amedumu klabuni hapo katika nafasi hiyo kwa miaka mitatu.

Kocha wa zamani wa PSG Mfaransa Laurent Blanc.

Safari ya aliyekuwa kocha Mfaransa wa PSG Laurent Blanc ndani ya timu ya matajiri hao wa jiji la Paris imehitimika hii leo baada ya klabu hiyo kutangaza rasmi kuachana na timu hiyo ambayo aliiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi 1 ya Ufaransa lakini haikuweza kufua dafu katika michuano ya Ulaya msimu huu.

Kuondoka kwa Blanc, beki wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Ufaransa, kunampa nafasi kocha wa zamani wa Sevilla, Unai Emery ambaye ndiye anayetarajiwa kuchukua nafasi hiyo.

Blanc aliteuliwa kuwa kocha wa PSG mwaka 2013 na kuingozia timu hiyo kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi 1, makombe mawili ya Coupe de France na ubingwa mara tatu wa kombe la Coupe de la Ligue.

Kuondoka kwake kunakuja baada ya Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi kunukuliwa akitoa kauli moja wiki chache zilizopita kuwa kutakuwa na mchakato wa kukijenga upya kikosi cha timu yao

Blanc ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia timu hiyo, Februari mwaka huu, anatarajiwa kulipwa euro milioni 22 ikiwa ni fidia ya kuvunjwa kwa mkataba wake.

Kuondoka kwa Blac kumekuja ikiwa ni siku chache tu kupia tangu klabu hiyo ilipomruhusu kuondoka ndani ya klabu hiyo mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic ambaye amemaliza mkataba wake.