Jumapili , 24th Apr , 2022

 Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa ameitaka klabu ya Simba kufanya vizuri kwenye mchezo wao wa mkondo wa pili dhidi ya Orlando Pirates kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho Afrika unaofanyika nchini Afrika Kusini.

(Waziri wa Michezo Mohamed Mchengerwa)

Akizungumza na wachezaji,benchi la ufundi na viongozi wa klabu ya Simba kwa njia ya simu ambapo amewatoa hofu kuhusu usalama kuelekea mchezo huo huku akiwataka wachezaji kwenda kushindana ili kuweza kulitangaza taifa kwenye michezo kimataifa.

“sisi kama wizara na serikali macho yetu yapo huko kwenu na mheshimiwa Rais anafatilia kwa karibu,kama wizara ndoto yetu inaweza kutimia kama nyinyi mkifanya vizuri huko.Twendeni tukimtanguliza Mungu mbele na wachezaji wekeni akili zenu uwanjani na msiwaze mambo ya nje ya uwanja na kama wizara tupo tayari kuja kuwapokea mkifanya vizuri”amesema Waziri Mchengerwa

Simba inashuka dimbani majira ya saa moja kamili usiku kwa saa za Afrika mashariki huku leo wakihitaji ushindi au sare yoyote kufuzu kwenda hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho barani afrika baada ya kupata ushindi kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa bao 1-0 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa mnamo April 17,2022