Jumamosi , 9th Jul , 2022

Klabu ya Simba SC ya Dar es salaam imemtangaza Habibu Kyombo kuwa mchezaji mpya wa klabu hiyo akitokea Mbeya Kwanza. Kyombo anakuwa mchezaji wa pili anasajiliwa na Simba SC msimu huu baada ya Moses Phiri.

Habibu Kyombo mshambuliaji mpya Simba SC

Msimu uliopita Habibu Kyombo alicheza michezo 12 ya Ligi Kuu Tanzania bara NBC Premier League akiwa na kikosi cha Mbeya Kwanza ambayo alijiunga nayo katika dirisha dogo la usajili na alicheza jumla ya dakika 1054 katika michezo hiyo na alifunga mabo 6 na alitoa pasi 1 ya kufunga bao (Assist).

Kyombo amewahi kuvichezea vilabu vya Mbao FC, Singida United na klabu ya Mamelodi Sundowns F.C. ya Afrika kusini. Inaripotiwa katika usajili huu Simba imelipa dau la Shilingi Milioni 35 kuipata saini ya mshambuliaji huyu.

Usajili wa kwanza wa Wekundu wa Msimbazi Simba katika dirisha hili la usajili ulikuwa wa mshambuliaji Moses Phiri raia wa Zambia lakini pia wachezaji wengine wanaotarajiwa kusajiliwa na klabu hiyo ni Lobi Manzoki, Shiza Kichuya, Nervé Ngombo na Augustine Okrah.