Jumapili , 4th Sep , 2022

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Saidi Yakubu ameiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya kirafiki ya Mpira wa Meza (Table Tennis) yaliyofanyika Septemba 04, Diamond Jubilee Dar es Salaam ambapo amesema, Tanzania na China zimekua mfano wa Mataifa rafiki Duniani.

Ujumbe wa Tanzania na China katika maadhimisho ya miaka 50 ya urafiki

Amesema, mchezo wa mpira wa meza ni miongoni mwa michezo inayokua hapa nchini, na Serikali inaendelea kuwekeza katika mchezo huo ambao unakuza vipaji na kutengeneza ajira kwa vijana.

"Mpira wa Meza unachezwa sana na wanafunzi katika shule za Msingi na Sekondari, na katika Mashindano ya Michezo kwa shule hizo pamoja na Vyuo vya Ualimu na Taasisi za Umma pia unachezwa na unaleta ushindani Mkubwa, hivyo ni miongoni mwa michezo inayotangaza nchi vyema" amesema Ndugu Saidi Yakubu.

Ametumia nafasi hiyo kuliagiza Baraza la Michezo nchini, kukaa na Ubalozi wa China kushirikiana na kuratibu kwa karibu zaidi matukio yote ya michezo yanayoshirikisha nchi hizo, ili kuweza kupata wachezaji wengi zaidi watakaoshindana.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Mhe. Chen Ming Jian  amesema China imedhamiria kujenga kiwanda Cha kuzalisha filamu, kubadilishana wataalamu katika sekta ya Michezo na Utamaduni na imeahidi kushiriki katika Tamasha la 41 la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo.

Mashindano hayo yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya  Umoja wa wacheza mpira wa Meza Tanzania na China pamoja na kituo cha Utamaduni cha China.