Jumapili , 9th Dec , 2018

Ni rasmi sasa, muda ambao mlinzi mpya wa klabu ya Simba, Zana Coulibaly ataanza kuonekana uwanjani umejulikana kwa mujibu wa kocha mkuu wa 'Wekundu hao wa Msimbazi, Patrick Aussems.

Mchezaji, Zana Coulibaly (kushoto), Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori (katikati) na Kocha, Patrick Aussems (kulia).

Mlinzi huyo raia wa Burkina Faso alisajiliwa mapema mwezi uliopita akitokea klabu ya Asec Mimosas ya Ivory Coast kwa lengo la kuisaidia klabu hiyo katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Klabu Bingwa barani Afrika baada ya kuumia kwa beki Shomari Kapombe.

Akizungumza juu ya muda wa mchezaji huyo kuanza kuichezea Simba, Aussems amesema kuwa hatoitumikia Simba katika michuano ya kimataifa mpaka pale watakapofanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Klabu Bingwa barani Afrika kutokana na kuzuiwa kuingiza majina mapya katika hatua za awali.

"Siwezi kumtumia hivi sasa katika michuano ya kimataifa kutokana na sheria kutubana, lakini tukitinga hatua ya makundi nitaanza kumtumia," amesema Aussems.

"Huku kwenye ligi watu wataanza kumuona katika mzunguko wa pili kwa sababu hapo atakuwa fiti zaidi na naamini atakuwa msaada mkubwa kwenye timu na kuziba pengo la Kapombe," ameongeza.

Simba hivi sasa inajiandaa kwaajili ya mchezo wa hatua ya pili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Nkana FC ya Zambia, Disemba 15, mchezo ambao Simba itaanzia ugenini nchini humo.

Pia katika kuelekea mchezo huo, klabu ya Simba imetoa nafasi kwa mashabiki wake wanaotaka kwenda kuishangilia timu yao nchini Zambia, ambapo jumla ya nauli ya kwenda na kurudi ikiwa ni Sh 130,000. Msafara ukitarajiwa kuanza Alhamisi ya wiki ijayo na kufika nchini Zambia Ijumaa, siku moja kabla ya mchezo huo utakaopigwa Jumamosi.