
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Naibu meneja wa kiwanda hicho, Shadrack Nsekela amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya wapangaji kushindwa kulipa madeni wanayodaiwa tangu mwaka 2015.
"Hakuna msalie mtume katika hili, tutawatoa wote bila kujali nani ni nani. Tumeanza kuwapa notisi tangu mwaka 2015 lakini hawalipi sasa tunawatoa," amesema Nsekela.
Amesema wapangaji waliopo katika kota za Urafiki jijini Dar es Salaam wanadaiwa kati ya Sh600 milioni na Sh1 bilioni. Nsekela amesema wameanza kuwatoa wapangaji wa ofisi, huku wale wa makazi wakitakiwa kujiandaa wakati wowote nao watatolewa.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya udalali ya Yono, Scholastika Kevela amesema baada ya siku 14 watapiga mnada mali walizokamata ili kufidia deni.