Jumatatu , 30th Aug , 2021

Klabu ya kongwe nchini, 'Dar es Salaam Young Africans' imefanikiwa kusheherekea tamasha lake la kilele cha wiki ya Mwananchi Jumapili ya jana Agosti 29, 2021 kwenye dimba la mkapa jijini Dar es Salaam kwa kupambwa na burudani mbalimbali na mchezo wa kirafiki dhidi ya Zanaco FC ya Zambia.

(Kikosi cha Yanga kilichoanza kwenye mchezo wa kirafiki kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi dhidi ya Zanaco FC kikitambulishwa mbele ya mashabiki zake kabla ya mchezo kuanza ambao baada ya kuchezwa Yanga walifungwa 2-1.)

Tamasha hilo huadhimishwa kila mwezi Agosti kila mwaka hufanywa kwa lengo la kuwaunganisha mashabiki na wanachama wa klabu hiyo, kuonesha wachezaji wapya waliosajiliwa pamoja na kufanya uzinduzi wa jezi mpya kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa mashindano.

Sherehe hizo zilizofanyika kwa aina ya pekee kwani mashabiki na wanachama wa klabu hiyo walijitokeza kwa wingi na kujaza uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 60, 000 wakiwa wameketi na kushuhudia michezo ya kirafiki ya utangulizi kabla ya mchezo dhidi ya Zanaco.

Mchezo wa kwanza wa utangulizi ni ule ulipwakutanisha Yanga U20 waliofungwa 3-1 dhidi ya Cambiasso Academy FC na baadaye timu ya wanawake ya Yanga, Yanga Princess ilishuka dimbani na kulazimishwa sare ya 1-1 na Ilala Queens huku zikisindikizwa na burudani kutoka kwa wanamuziki.

Koffi Olomide Mopao kutoka DR Congo ndiye aliyekuwa mwanamuziki mahsusi kutumbuiza kwenye tamasha hilo na alifanya hivyo mishale ya jioni na kuwaburudisha mashabiki na wanachama wa klabu hiyo pamoja na wageni wote waalikwa.

Mishale ya saa 12 jioni, Mgeni rasmi wa tamasha hilo, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Selemeni Abdulla ambaye aliwahutubia wananchi kwa kuwasihi wawe wamoja na kumaliza makando kando yao huku akiwa na imani Yanga itakuwa mabingwa kutokana na usajili walioufanya.

Baada ya Hotuba ya mgeni rasmi, mchezo wa kirafiki maalum wa kupamba tamsha hilo ulichezwa ambapo Yanga walicheza na Zanaco ya Zambia na kufungwa mabao 2-1 licha ya kusheheni wachezaji wake wapya kasoro Khalid Aucho ambaye yupo kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Uganda.

Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Heritier Makambo dakika ya 30 kabla ya Ackim Mumba dakika ya 66 na bao la ushindi la Zanaco FC likafungwa na Kelvin Kapumbu dakika ya 76 mshale ambao ulimshinda mdaka mishale mahiri Djigui Diarra mlinda mlango mpya wa klabu ya Yanga.

Baada ya mchezo huyo kumalizika na tamasha kutamatika kwa shangwe, Kocha msaidizi wa Yanga, Razak Siwa amesema wanayanga wasiwe na mashaka yeyote kwani wamesajili wachezaji bora lakini wapo kwenye hali ya ujenzi wa timu hivyo kila kitu kitakuwa sawa siku za usoni.