
Waandamanaji 33 waliouawa wakati wa maandamano ya kupinga ufisadi nchini Nepal mwezi huu wanasemekana kupigwa na risasi za moja kwa moja zilizofyatuliwa na polisi kwa mujibu wa taasisi ya matibabu iliyofanya uchunguzi wa maiti hizo.
Matokeo yaliyotolewa na mjumbe wa idara ya dawa ya uchunguzi wa Taasisi ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Tribhuvan, ambaye ameiambia Reuters kwa sharti la kutotajwa jina amelithibitisha hilo na kuwa uthibitisho wa kwanza rasmi kwamba risasi za moto zilitumika wakati wa machafuko hayo, ambapo watu 74 waliuawa na zaidi ya elfu mbili kujeruhiwa.
Uchunguzi huo wa maiti ulifanyika katika kampasi ya matibabu ya Maharajgunj yenye makao yake mjini Kathmandu, ambayo ilipokea miili 47 kutoka hospitali katika mji mkuu baada ya maandamano. Picha ambazo hazijathibitishwa za risasi zisizo za mpira na waandamanaji waliokuwa na majeraha kichwani na kifuani zilikuwa zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii baada ya maandamano yaliyoongozwa na Gen-Z kupinga mfumo wa ufisadi nchini humo.
Mjumbe huyo wa idara ya uchunguzi wa kitabibu alisema kati ya miili 34 yenye majeraha ya risasi iliyofanyiwa uchunguzi, kumi ilipigwa kichwani, 18 kifuani, 4 tumboni na miwili shingoni. Mtu mmoja tu ndiye aliyepigwa na risasi ya mpira. Idara haikuweza kubaini kiwango cha risasi hizo au aina mahususi ya bunduki iliyotumiwa kurusha risasi hizo.
Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imetoa wito wa uchunguzi wa haraka na wa uwazi" juu ya tuhuma za matumizi yasiyo ya lazima au yasiyo na uwiano ya vikosi vya usalama wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na makundi ya vijana.
Serikali ya mpito inayoongozwa na jaji mkuu wa zamani Sushila Karki mwenye umri wa miaka 73 imeunda jopo la kuchunguza ghasia hizo. Karki, ambaye ni mwanamke wa kwanza mkuu wa serikali ya Nepal, amesema atarekebisha kushindwa kwa serikali na kukabiliana na ufisadi, huku pia akisaidia kuunda nafasi za kazi na kuinua viwango vya maisha. Uchaguzi umetangazwa Machi 5, lakini wataalam wamesema anaweza kuongeza muda wake kutokana na uwepo wa changamoto kubwa katika taifa hilo.