Monday , 22nd Feb , 2016

Chama Cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA) kimesema idadi kubwa ya wanawake wanaokwenda katika vituo vya afya nchini mara baada ya mimba kuharibika ni wale waliotoa mimba katika njia zisizo salama na kuhatarisha maisha yao.

Akiongea leo jijini Dar es salaam, Afisa Uchechemuzi na Utetezi wa TAWLA, Sima Bateyunga amesema kutokana na hali hiyo zaidi ya asilimia 16 ya wanawake wanapoteza maisha mara baada ya kufika katika vituo vya afya kutokana na kutoa mimba kwa njia zisizo sahihi ikiwa ni pamoja na kwa waganga wa kienyeji.

Kwa upande wake, daktari Bingwa wa Magonjwa ya akina mama na uzazi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Ali Said amesema hali hiyo inaathiri kwa kiwango kikubwa via vya uzazi kwa wanawake huku wengi wao wakipoteza maisha kutokana na kuwatumia madaktari wasiokuwa na sifa.