
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk, Charles Msonde aliyedai kuwa lengo la baraza hilo ni kujiridhisha katika takwimu ambazo zilitumika katika vyeti hivyo kwa mfumo wa GPA na si kubadili matokeo.
''Vyeti hivi baraza limevigawa hivi karibuni na lilichofanya sasa limezuia kwanza shule zisigawe mpaka litakapotoa maelekezo mengine, msingi huo wa kuzuia uko kwenye hoja ya kuhakikisha tu kwamba linajiridhisha kwenye takwimu zake kama zimekaa sawasawa katika vyeti vilivyokwenda kila shule'' Amesema Msonde
Aidha zoezi hili halitawaathiri wanafunzi ambao wapo nje ya nchi na endapo baraza hilo litahitaji cheti chochote litawasiliana na wahusika.
Ikumbukwe kuwa baada ya waziri wa elimu Dkt Joyce Ndalichako kupewa nafasi na Rais Dkt. John Magufuli alitangaza kusitishwa kwa mfumo wa kusahihisha matokeo kwa GPA na badala yake mfumo wa Division uweze kurejeshwa ambapo matokeo ya kidato cha nne yametoka kwa mfumo huo.