Monday , 2nd May , 2016

Maafisa mjini Nairobi nchini Kenya wamesema idadi ya watu waliokufa baada ya jengo la makaazi kuporomoka katika mtaa wa Huruma imefikia watu 16 na wengine 73 bado hawajapatikana.

Watu wakiendelea na Uokozi katika jengo lililoanguka Nairobi

Shughuli za uokozi bado zinaendelea kujaribu kuwapata manusura wa mkasa huo. Jengo hilo la ghorofa sita lilianguka siku ya Ijumaa jioni kufuatia mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha mjini Nairobi.

Awali maafisa wa idara ya kukabiliana na majanga walisema idadi ya waliofariki ilikuwa 12 na 135 walijeruhiwa. Jengo hilo lililoporomoka Huruma lilikuwa ni makaazi ya zaidi ya familia 150.

Jumla ya watu 23 wamekufa mjini Nairobi kutokana na mafuriko.

Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi iligunduwa asilimia 58 ya majengo katika mji mkuu Nairobi hayafai kuishi watu kutokana na baadhi ya wajenzi kukiuka sheria ili kukamilisha haraka miradi ya ujenzi kukidhi mahitaji makubwa ya nyumba mjini Nairobi.