Thursday , 6th Oct , 2016

Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Aksoni amesema serikali itahakikisha inasimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa inayohusu maslahi ya watu wenye ulemavu wa macho ili kuwawekea mazingira rafiki ya upatikanaji wa elimu na ajira nchini.

Maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu wa macho (siku ya fimbo nyeupe) mkoani Tabora (Siku za nyuma)

Dkt. Acksoni ameyasema hayo mkoani Mbeya ambako alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya fimbo nyeupe ambapo amesema Bunge la Tanzania litahakikisha linaisimamia serikali ili itekeleze mikataba na utekelezaji wa sheria na sera za walemavu.

Amesema kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha haki na maslahi ya walemavu hususani kwa wasioona yanalindwa na kwamba itaendelea kuboresha mazingira ya shule ili watu wenye ulemavu wa macho waweze kupata huduma bora itakayoendana na ushindani wa ajira.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa macho (TLB), Luis Benedictor amesema kundi hilo limekuwa likikumbana na vikwazo vya kupata ajira kutoka sekta binafsi na serikalini licha ya kuwa na sifa na vigezo vya kuajiriwa.

Aidha Benedictor ameitaka jamii kuwajibika kwa kuwapeleka watoto wenye ulemavu wa macho shuleni ili kundi hilo liwe na wasomi ambao wataingia kwenye soko la ajira wakati Tanzania ikijiandaa kuwa nchi ya viwanda mwaka 2020.