Monday , 29th Feb , 2016

Klabu ya soka ya Azam imekamilisha idadi ya timu nane za kucheza Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufuatia ushindi wa bao 2-1 dhidi ya wenyeji, Panone FC jioni ya leo uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Kilimanjaro.

Panone walitangulia kuandika bao la kichwa likiwekwa kambani na beki wake Godfrey Mbuda aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki kulia, Ayoub Masoud dakika ya 48.

Hata hivyo, beki Serge Wawa Pascal akafuta makosa ya safu ya ulinzi kwa kuisawazishia Azam FC dakika ya 64 akimalizia kwa kichwa kona ya beki wa kulia, Erasto Nyoni kabla ya Allan Wanga kupigilia msumari dakika ya 77 akiunganisha kona ya Erasto nyoni.

Azam FC sasa inaungana na Yanga, Simba, zote za Dar es Salaam, Ndanda FC ya Mtwara, Coastal Union ya Tanga, Geita Gold ya Geita, Mwadui FC ya Shinyanga na Prisons ya Mbeya kutinga Nane Bora.