Saturday , 10th Jun , 2017

Msanii Darassa aliyetamba na ngoma ya 'Muziki' anatarajiwa kutumbuiza kesho katika mechi ya fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Rapa Darassa.

Darassa ambaye ana ngoma nyingi zinazofanya vizuri ikiwemo 'Hasara Roho' aliyoiachia siku za hivi karibuni, tayari amethibitisha kutumbuiza katika fainali hiyo ambayo itawakutanisha "mashemeji derby" kutoka Kenya.

"Jumapili hii ya tarehe 11, usikose pale katika viwanja vya uhuru kwenye SportPesa Super Cup nitakuwepo pale mapema kabisa kuanzia saa 6 mchana" alisema msanii huyo.

Fainali hiyo itakutanisha vilabu kutoka nchini Kenya ambavyo ni Gor Mahia na AFC Leopards, baada ya klabu zote nne za Tanzania kutolewa katika michuano hiyo.

Mshindi wa fainali hiyo atacheza mechi dhidi ya klabu kutoka Uingereza Everton.