Tuesday , 27th Nov , 2018

Klabu ya soka ya Mbabane Swallows, imesema inajivunia kuja kucheza tena hapa Tanzania, ikiwa ni mara yao ya pili baada ya Machi 12, 2017 kucheza na Azam FC na kufungwa bao 1-0, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Kikosi cha Mbabane Swallows

Akiongea leo na wanahabari kwenye makao makuu ya shirikisho la soka nchini TFF, kocha mkuu wa Mbabane Swallows, Thabo "Koki" Vilakati, amesisitiza baada ya kurudi tena Dar es salaam kila mtu atakuwa anajua wamefuata nini.

''Tunashukuru tumefika hapa salama usiku wa leo, tunaamini tutakuwa na mchezo mgumu kwasababu Simba ni timu nzuri ila tunajua pia wao wanajua tumerudi hapa kwa mara nyingine kwahiyo tunachokitarajia wanakijua'', amesema Koki.

Msimu uliopita Mbabane Swallows ya Swaziland ilitinga hatua ya makundi kwa kushinda kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya Zanaco ya Zambia.

Mbabane iliishia hatua hiyo ya makundi ambapo timu za Primeiro Agosto ya Angola na Etoile du Sahel ya Tunisia zilitinga robo fainali na kuziacha Mbabane na Zesco United.

Mchezo wa Simba na Mbabane utachezwa kesho kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam saa 10:00 mchana.