Tuesday , 10th May , 2016

Mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kati ya wenyeji Ndanda FC na Yanga uliokuwa ufanyike Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara sasa utafanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Afisa habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) Alfred Lucas amesema, Bodi ya Ligi imeridhia maombi hayo mara baada ya Ndanda na Yanga kushawishiana na kufikia makubaliano ya mchezo huo ambao hapo awali ulitakiwa kuchezwa Mei 15 baadaye ukarudishwa mpaka Mei 14 na wakaamua tena uchezwe Mei 13 Uwanja wa Nang'wanda mjini Mtwara lakini hivi sasa rasmi utachezwa Mei 14 Uwanja wa Taifa.

Lucas amesema, makubaliano hayo yameafikiwa baada ya timu ya Yanga kuiomba Ndanda FC mechi ichezwe Dar es Salaam kwa sababu wanataka kuwahi Angola Mei 17 kucheza na wenyeji Sagrada Esperanca katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Lucas amesema, Ndanda wamekubali kucheza mechi zote mbili za msimu na Yanga ugenini, kwa sababu hawana cha kupoteza wala kupata zaidi katika Ligi Kuu ilipofikia ukingoni.

Katika mchezo huo, Yanga itakabidhiwa Kombe lake la ubingwa wa Ligi Kuu iliyojihakikishia Jumapili baada ya Simba SC kufungwa bao 1-0 na Mwadui FC katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa upande mwingine Lucas amesema, mechi za mwisho za kufunga dimba la Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara zilizotakiwa kupigwa Mei 21 mwaka huu zimesogezwa mbele kwa siku moja na zitachezwa Mei 22 mwaka huu ili kuipa Yanga nafasi ya kuweza kupumzika atakapotokea kutoka nchini Angola.

Lucas amesema, Yanga wanatarajia kukutana na Esperanca Mei 17 mwaka huu na Mei 21 ndio zilikuwa zichezwe mechi za kufunga pazia la Ligi ambapo Yanga ingetakiwa kusafiri mpaka Songea kucheza dhidi na Majimaji hivyo bodi ya Ligi ikaridhia kuwa michezo yote imalizike Mei 22 mwaka huu ili kuipa Yanga nafasi ya kuweza kupumzika.